Alhamisi 21 Mei 2026 - 23:30
Mafungamano ya Waislamu ni miongoni mwa malengo ya faradhi ya Hija

Hawza/ Mwalimu na mwanaharakati wa kitamaduni kutoka Iraq anaamini kwamba, Mwenyezi Mungu kupitia faradhi hii ya Kiungu anataka kuwakaribisha Waislamu wao kwa wao na kuwafanya kuwa mwili mmoja wenye nguvu na ustahiki, kwa sababu mkusanyiko na umoja wao ni dhihirisho la heshima na nguvu yao.

Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Habari la Hawza, Muna Adib, mwalimu na mwanaharakati wa kitamaduni kutoka Iraq, katika kikao maalumu cha “Hija; Mahali pa Miadi ya Umoja” kilichofanyika Jumatano kwa juhudi za Majma' al-'Alami li-Taqrib al-Madhahib al-Islamiyyah, huku akirejelea aya ya 27 ya Suratul-Hajj:

"Na watangazie watu Hija; watakujia kwa miguu na juu ya kila ngamia aliye konda, wakija kutoka katika kila njia ya mbali."

alisema: “Uislamu ulikuja ili uwe njia ya saada ya dunia mbili, ulikuja kubeba ujumbe wa uongofu na marekebisho pamoja na bendera ya uhuru na uadilifu.”

Aliendelea kusema: “Miongoni mwa sifa kuu kabisa za Uislamu ni kwamba uliinua hadhi na cheo cha mwanadamu na ukamfanya kuwa khalifa wa Mwenyezi Mungu na mbora wa viumbe ili aijenge dunia kwa ustaarabu na imani, pale ulipomtukuza kwa faradhi, ukamuamrisha majukumu ya kisharia, na kumfaradhishia Swala, Saumu, Jihadi na Hija.”

Adib aliitaja Hija kuwa ni moja ya nguzo tano za Uislamu na akaongeza: “Hija ni miongoni mwa ibada kubwa zaidi za Kiislamu ambazo Mwenyezi Mungu amewajibisha kwa kila Muislamu mwenye uwezo wa kimwili na kifedha; ni faradhi ambayo Mwenyezi Mungu ameiweka ili umma wa mwisho wa Mitume uendelee kuinua bendera ya Tawhidi na kuhuisha umoja wa kibinadamu. Faradhi hii ya kila mwaka si safari ya kiroho na ibada za kimila pekee, bali ni mradi wa kimapinduzi wa kumbadilisha mtu binafsi na kuujenga umma, na ni wajibu wetu kutafakari juu yake, hasa wakati ambapo umma wa Kiislamu unapitia nyakati zake ngumu na hatari zaidi.”

Mwanaharakati huyu wa kitamaduni wa Kiiraq alikumbusha kuwa: “Hakika Hija ni nembo ya umma wa Kiislamu; ni alama ya kidini inayoweza kuupatia umma wa Kiislamu mkusanyiko wa maarifa yanayopatikana kupitia ibada za Hija, Hija ndiyo faradhi pekee ambayo Mwenyezi Mungu amewaita Waislamu wote kuitekeleza kwa wakati mmoja na katika sehemu moja ili Waislamu waunganishwe katika siku maalumu kuelekea lengo moja, kwa hiyo; uwepo wa Waislamu katika msimu wa Hija lazima uwe na lengo na maana yake ya kweli; si utajo wa Mwenyezi Mungu na ibada pekee.”

Aliitaja Hija kuwa ni fursa ya kipekee ya kuunda umoja kati ya mataifa ya Kiislamu na akasema: “Waislamu kutoka sehemu za mbali kabisa duniani huja katika eneo hili takatifu kwa mapenzi ya Al-Kaaba, kwa ajili ya kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu, kujitenga na maadui wa Mwenyezi Mungu, kufahamiana wao kwa wao na kutambua maumivu ya wenzao. ‘Hija’ ni nguzo kuu ya maisha ya umma mmoja, kwa sababu ndani yake mataifa ya Kiislamu huhisi uwepo wa ‘Umma wa Muhammadi’, Wanahisi undugu, ukaribu, nguvu na umoja.”

Adib alikumbusha kwamba; katika msimu huu ni lazima masuala muhimu ya ulimwengu wa Kiislamu yazungumzwe, kwa sababu licha ya juhudi za istikbari kuficha ukweli wa jinai zake, ni wajibu kwa kila Muislamu kutekeleza jukumu lake la kuwaelimisha wengine; kwa sababu Mwenyezi Mungu kupitia faradhi hii ya Kiungu anataka kuwakaribisha Waislamu wao kwa wao na kuwafanya kuwa mwili mmoja wenye nguvu na ustahiki, kwani mkusanyiko na umoja wao ni dhihirisho la heshima na nguvu yao.

Mwanaharakati huyu wa kitamaduni alieleza kuwa “umoja” na “utambulisho mmoja wa Kiislamu” ndilo jambo linaloufanya ubeberu ushindwe kuunda pengo kati ya mataifa ya Kiislamu.

Alisisitiza kuwa: Leo ulimwengu wa Kiislamu unapokea mapigo makali kutokana na kupuuza hazina hii kubwa ya Kiungu, kiasi cha kwamba jamii za Kiislamu zimechukua sura ya mgogoro na maangamizi, kwa masikitiko, leo ulimwengu wa Kiislamu umeghafilika na Mwenyezi Mungu, kutokujali hatima ya umma wa Kiislamu, na kutokuwa macho mbele ya njama za maadui wa Uislamu na Waislamu.

Kwa sababu lengo la ubeberu ni kuunda hitilafu na migogoro kati ya Waislamu, kwa sababu hiyo, Mwenyezi Mungu amejaalia “kujiepusha na washirikina” kuwa sehemu ya Hija na nguzo yake ya msingi:

"Na ni tangazo kutokana na Mwenyezi Mungu na Mtume wake kwa wote siku ya Hija Kubwa kwamba Mwenyezi Mungu na Mtume wake hawana jukumu lolote kwa washirikina"

Adib alisisitiza kwamba; ni wajibu kwa mataifa kutangaza kujitenga kwao na maadui wa ulimwengu wa Kiislamu, yaani Marekani muuaji wa watoto na Israel mwenye kumwaga damu katika hilo, Imam Khomeini alifanya juhudi zenye athari kubwa katika kuifafanua sura bora na sahihi ya faradhi hii inayozalisha umoja na kuleta heshima, na ni kwa baraka za juhudi hizo ndipo Waislamu wamepata ujasiri wa kukabiliana na kambi inayoupinga Uislamu.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha